Messi afunga hat-trick ya 50 katika ushindi wa Barca

Ni mchezaji ambaye moyo wake wote uko dimbani Nou Camp na kwa kiasi kikubwa kutokana na ukweli kwamba Barcelona ndio timu iliyompa nafasi ya kuwa mchezaji ambaye mpaka sasa baadhi wanasema sio binaadamu. Kwamba ni kiumbe kutoka sayari nyingine. Na kwa kiasi kikubwa mashabiki waliofika uwanjani na sio tu wa ugenini bali pia wa nyumbani wanaweza kuridhika na mambo waliyoyaona kutoka kwa nyota huyo.

Namzungumzia Lionel Messi. Muargentina huyo alifunga hat trick ya 50 ya taaluma yake wakati Barcelona ilitoka nyuma na kuibamiza Sevilla 4 – 2 na kutanua mwanya wao kileleni mwa La Liga hadi pointi 10.

Katika mambo yake tunayayofahamu uwanjani, nahodha huyo wa Catalans alisawazisha bao la kwanza kwa kusukuma wavuni kombora kutoka hatua 16. Alisawazisha kwa mara ya pili kwa kufunga bao safi kutokea pembeni ya kisanduku cha hatari.

Messi kicha akamvisha kanzu kipa Tomas Vaclik kwa kufunga lake la tatu na la 36 katika mechi 35 dhidi ya Sevilla, kabla ya kumuandalia pasi Luis Suarez katika dakika za majeruhi ili kufunga kazi kwa kuweka kambani bao la nne.

Kwa kiasi kikubwa ilikuwa mechi ya maonyesho ya mchezaji mmoja kwa sababu Barcelona haikuonekana kuwa na mchezo wa kuridhisha licha ya kurefusha uongozi wao kileleni dhidi ya nambari mbili Atletico Madrid, ambao watawaalika Villarreal Jumapili.

Sevilla – ambao fomu yao sio nzuri – walitangulia kufunga bao katika kipindi cha kwanza kupitia Jesus Navas kutokana na shambulizi la kuvizia kabla ya Gabriel Mercado kusukuma wavuni la pili kutoka hatua nane.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends