Messi aisaidia Barcelona kuizamisha Liverpool Nou Camp

Liverpool watalazimika kukaza buti katika uwanja wao wa Anfield baada ya Barcelona kuwachabanga 3 – 0 katika ngome yao ya Nou Camp katika mechi ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya kombe la vilabu bingwa Ulaya.

Baada ya kujipata nyuma kupitia bao la Luis Suarez katika kipindi cha kwanza, wachezaji wa Jurgen Klopp walionekana kutawala mpira na kuwa na uwezo wa kusawazisha huku Mohamed Salah na James Milner wakimjaribu kipa Marc-Andre ter Stegen wa Barcelona.

Hata hivyo Barcelona walionyesha kwamba wana uwezo mkubwa kwa kuizuia Liverpool katika lango lao.

Na haikuchukua muda kabla ya Messi kuongeza uongozi wa Barcelona baada ya shuti la Suarez kugonga mwamba wa goli kabla ya Messi kufunga bao la pili.

Lakini ni bao lake la pili ambalo liliiunyanyua uwanja mzima. Alifunga bao tamu kupitia mkwaju wa freekick kutoka umbali wa karibu hatua 35. Sasa Liverpool watalazimika kuonyesha muujiza Jumanne wiki ijayo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends