Messi atupia mbili kambani Barca ikiinyeshea Real Betis 5 – 2

Staa wa Barcelona Lionel Messi akitokea katika mbao za akiba amekisaidia kikosi cha timu hiyo kushinda mechi ya kwanza ndani ya La Liga katika mechi tano zilizopita.

Katika mchezo huo, Barcelona imeiadhibu Real Betis kwa goli 5-2 huku mshambuliaji staa Lionel Messi akifunga bao lake la kwanza lisilo la mpira wa kutengwa (tuta). Ousmane Dembele aliwapa utangulizi Barca kwa juhudi za kipekee kabla ya penati ya Antoine Griezmann kuokolewa na mlinda mlango wa Betis.

Antonio Sanabria akasawazisha dakika chache kabla ya mapumziko. Lakini Messi alipoingia ungwe ya pili alisababisha goli la Griezmann na kufunga mawili mwenyewe kabla ya bao la tano kufungwa na kinda Pedri.

Yalikuwa matokeo hitajika sana kwa kocha Ronald Koeman ambaye kikosi chake kimeanza kwa kusuasua katika msimamo wa ligi baada ya kuvuna alama mbili pekee kwenye mechi nne za mwisho za La Liga.

Matokeo hayo yanaifanya Barcelona kukwea mpaka nafasi ya nane kwenye msimamo wa La Liga alama moja nyuma ya Real Betis.

Author: Bruce Amani