Messi awapiku Ronaldo, Neymar Jr kwa kuingiza mpunga

275

Mshambuliaji wa FC Barcelona Lionel Messi amewapiku staa wa Kireno Cristiano Ronaldo na wa Kibrazil Neymar Jr kwa wanasoka wanaolipwa zaidi duniani kwa mwaka 2020.

Takwimu hizo ambazo zimetolewa na jarida la Forbes zimemtaja staa wa Argentina Lionel Messi kuwa nambari moja huku Ronaldo akikamata nafasi ya pili wakati mlinda mlango wa Hispania na Manchester United David de Gea akikamilisha 10 bora ya wanaolipwa zaidi.

Forbes imemkadiria Messi kuwa kwa mwaka anaingiza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 97.2 wakati fowadi wa Juventus Cristiano Ronaldo anavuna kiasi cha dola za Kimarekani milioni 90.3 na kuwa mtu wa pili.

Neymar amewekwa nafasi ya tatu kwa wanasoka wanaolipwa zaidi na kinda wa Kifaransa Kylian Mbappe amekamata nafasi ya nne.

Wachezaji watatu waocheza Ligi Kuu nchini England wametajwa kwenye orodha hiyo ambapo kiungo mshambuliaji wa Manchester United Paul Pogba, winga wa Misri na Liverpool Mohammed Salah na David de Gea wakiwa wameingia huko.

Orodha ya tatu bora imejirudia tena baada ya mwaka 2019 kuwa sawa na hiyo ingawa staa wa PSG Mbappe amepanda nafasi tatu kutoka saba hadi nne.

Orodha kwa ujumla imekaa hivi kwa wanasoka wanaolipwa zaidi kwa mujibu wa Forbes.

  1. Lionel Messi (Barcelona na Argentina) anapata pauni milioni 97.2.
  2. Cristiano Ronaldo (Juventus na Ureno) anapata pauni milioni 90.3.
  3. Neymar (Paris St-Germain na Brazil) anapata pauni milioni 74.1.
  4. Kylian Mbappe (Paris St-Germain na Ufaransa) anapata pauni milioni 32.4.
  5. Mohamed Salah (Liverpool na Misri) anapata pauni milioni 28.5.
  6. Paul Pogba (Manchester United na Ufaransa) anapata pauni milioni 26.2.
  7. Antoine Griezmann (Barcelona na Ufaransa) anapata pauni milioni 25.5.
  8. Gareth Bale (Real Madrid na Wales) anavuna pauni milioni 22.4.
  9. Robert Lewandowski (Bayern Munich na Poland) anavuna pauni milioni 21.6.
  10. David de Gea (Manchester United na Hispania) anapata pauni milioni 20.8.

Author: Asifiwe Mbembela