Messi aweka historia wakati Barca ikishinda Prague

Lionel Messi aliisaidia Barcelona kupata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Slavia Prague na kukamata usukani wa Kundi F katika Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku. Messi amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika misimu 15 mfululizo ya Champions League. Alifunga bao la kwanza na kutoa pasi ya bao la pili katika ushindi huo mwembamba mjini Prague.

Liverpool iliizidi nguvu Genk yake Mbwana Samatta kwa kuibamiza mabao 4 – 1. Samatta alifunga bao la kichwa lakini likafutwa na VAR kwa sababu lilikuwa la kuotea.

Liverpool iko nyuma ya Napoli na pengo la pointi moja katika Kundi E baada ya klabu hiyo ya Italia kupata ushindi wa 3 -2 dhidi ya RB Salzburg. Inter Milan na Borussia Dortmund zipo nyuma ya Barca na pengo la pointi tatu. Inter iliizaba Dortmund 2 – 0 katika mechi nyingine ya Kundi F.

Mapema jana, Chelsea ilipata ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Ajax na kuliweka wazi Kundi H. Matokeo hayo yana maana zote mbili zina pointi 6. Valencia ina nne baada ya kutoka sare na Lille. Klabu ya Ujerumani RB Leipzig inaongoza Kundi G na pointi 6 baada ya kuibwaga Zenit St Petersburg 2 – 1. Lyon walipoteza 2 – 1 dhidi ya Benfica.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends