Mesut Ozil awaachia ujumbe mzito Arsenal baada ya kutemwa katika kikosi cha klabu hiyo

Kiungo mshambuliaji wa Arsenal Mesut Ozil amesema timu hiyo imemkatisha tamaa baada ya kuachwa kando katika majina 25 ya wachezaji wa klabu hiyo watakaocheza Ligi Kuu nchini England. Ozil, 32, ambaye alijiunga na timu hiyo mwaka 2013 kwa ada ya pauni milioni 42.4 hajagusa mechi za ushindani za Arsenal tangu mwezi Machi. Pengine ni wakati mgumu zaidi kwake baada ya kuwekwa kando pia kwenye kikosi cha wachezaji 23 ambao wanatakiwa kucheza michuano ya Ligi ya Europa.

Mkataba wa Ozil unafikia tamati mwishoni mwa msimu 2021. Baada ya kufungiwa nje, Mesut Ozil kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani na Madrid ameandika ujumbe wenye simanzi kwa mashabiki wa timu hiyo, alisema “Utu katika nyakati hizi hauthaminiki hata kidogo”. “Imeniumiza jina langu kutojumuishwa kwa wachezaji wa Arsenal watakaocheza EPL”.

“Mara zote nimekuwa nikifanyiwa visivyo hapa lakini nilisalia katika mtazamo chanya wiki hadi wiki katika klabu ambayo naipenda zaidi, nitaendelea kujituma uwanja wa mazoezi labda naweza kurudishwa kwenye kikosi”.

Tangu alipojiunga na Arsenal akitokea Real Madrid miaka saba iliyopita, Ozil amefunga goli 44 katika mechi 254 katika mashindano yote ndani ya uzi wa The Gunners.

Author: Bruce Amani