Michezo ya Olimpiki Tokyo yaahirishwa hadi 2021

Mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020 yameahirishwa hadi msimu wa joto mwaka wa 2021 kwa sababu ya janga la virusi vya corona linalouyumbisha ulimwengu. Hayo yametangazwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC. Michezo hiyo ilipangwa kufanyika Julai 24 hadi Agosti 9, lakini baada ya mashauriano ya simu kati ya rais wa IOC Thomas Bach na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, uamuzi wa pamoja wa kihistoria ukachukuliwa kwa mara ya kwanza kuahirisha Olimpiki katika wakati wa amani. Abe amesema Bach alikubaliana kwa asilimia 100 wakati Japan iliiomba IOC kuisogeza mbele michezo hiyo. Katika taarifa ya pamoja, Japan na IOC zimesema kuwa kwa kuzingatia habari ya sasa ya Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO, Michezo ya Tokyo lazima ipangwe upya na kuandaliwa 2021, ili kulindfa afya ya wanamichezo, kila mmoja anayehusika na Tamasha hilo na jamii ya kimataifa.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments