Kandanda la wanawake kutinga Olimpiki 2020 kutimua vumbi

Mzunguko wa nne kufuzu katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika nchini Japan mwaka 2020 kwa upande wa wanawake barani Afrika, inachezwa mwishoni mwa wiki hii.

Mataifa yanayowania nafasi hiyo ni pamoja na Kenya, Zambia, Cameroon na Ivory Coast. Harambee Starlets ya Kenya itachuana na The She-polopolo ya Zambia katika mchuano wa mzunguko wa kwanza, mechi itakayochezwa Ijumaa jioni jijini katika uwanja wa Kimataifa wa soka wa Kasarani jijini, Nairobi.

Siku ya Jumamosi, Ivory Coast itamenyana na Cameroon katika uwanja wa Treichville, jijini Abidjan. Mechi hizi zinachezwa nyumbani na ugenini na mshindi atafuzu katika hatua ya mwisho, mechi zitakazopigwa nyumbani na ugenini mwezi Januari mwaka 2020.

Timu itakayoshinda ndiyo itakayofuzu lakini, ikayoshindwa itachezwa na mwakilishi aliyemaliza katika nafasi ya pili kutoka bara la Amerika Kusini CONMEBOL.

Author: Bruce Amani