Mikiki mikiki ya TPL kurejea baada ya michuano ya kimataifa

236

Ligi kuu ya kabumbu nchini Tanzania inarejea tena viwanjani baada ya mapunziko ya siku kadhaa kupisha michuano ya kimataifa kwa timu za taifa kuwania kufuzu kwa AFCON 2019 nchini Cameroon

Kesho Ijumaa Oktoba 19 nyasi za viwanja vitatu zitumia ambapo timu sita zitashuka dimbani kusaka pointi tatu muhimu ili kujizatiti na kujiweka vyema katika msimamo wa ligi kuu msimu huu.

Vinara wa ligi waoka mikate wa Azam FC saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki watakua katika dimba lao la nyumbani la Azam Complex kuwakaribisha African Lyon, lakini mapema hapo kesho kutakua na michezo miwili, katika uwanja wa Nangwanda Sijaona ambapo wenyeji wa uwanja huo Ndanda FC watavaana na timu ya Mbeya City,

Timu ya wachimba madini huko Shinyanga Mwadui FC watakua katika uwanja wa Mwadui Complex kujaribu bahati yao dhidi ya Ruvu Shooting toka mkoa wa Pwani

Jumamosi ya Oktoba 20 2018 kutapigwa mechi tatu, mchezo wa kwanza utapigwa Mchana majira ya saa nane kwa Maafande wa Tanzania Prisons watakapowakaribisha Singida United ya Singida katika uwanja wa Kumbu Kumbu ya Sokoine mjini Mbeya,

Wagosi wa Kaya Coastal Union na JKT Tanzania ya Dar es Salaam mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabingwa wa kihistoria Yanga SC watakuwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza.

Mabingwa watetezi, Simba SC  waatateremka dimbani siku ya Jumapili kuwakaribisha Stand United Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ukitanguliwa na mchezo wa Lipuli FC wakiwakaribisha Kagera Sugar ya Bukoba Saa nane mchana Uwanja wa Samora mjini Iringa na Mbao FC watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro Saa kumi jioni mchezo huu utanguruma katika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.

Author: Bruce Amani