Milan yamtimua kocha wake Giampaolo

90

AC Milan imemfukuza kocha Marco Giampaolo baada ya kuifundisha timu hiyo miezi mitatu na nusu kutokana na mwanzo mbaya wa matokeo ya ligi Kuu Serie A. Milan inakamata nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo alama tatu juu ya mstari wa kuangukia katika timu zinazojikwamua kushuka daraja.

Giampaolo, 52, alichukua virago vya Gennaro Gattuso mwezi Juni ameshinda mechi tatu kati ya saba za Seria A. Wakati Marco anafurushwa tayari jina la bosi wa zamani wa Inter Milan Stefano Pioli limehusishwa na kazi hiyo lakini mashabiki hawajaafiki bado.

Licha ya kuhusishwa kujiunga na mabingwa hao wa Ligi ya mabingwa lakini mashabiki wa Milan wameonyesha kutokubaliana na kocha anayehusishwa kwenda Milan, hivyo wameanzisha “Hashtag” mtandaoni inayoenda kwa #PioliOut kuashiria kutokubaliana na Pioli hata kabla ya kujiunga.

“Kila mmoja wetu alifurahia kufanya kazi na Marco, lakini tunamtakia kila la heri katika kazi yake” taarifa rasmi kutoka AC Milan ilieleza. Vipigo vitatu kutoka kwa mpinzani wake Inter, pamoja na Torino na Fiorentina vimetajwa kama kaa la moto kwa Marco ambaye pia msimu uliopita alikuwa Sampdoria.

Anguko la kiuchumi limeelezwa kama changamoto kubwa kwa mabingwa hao mara 8 wa Ulaya ambao tangu mwaka 2011 haijawai twaa taji lolote.

Author: Bruce Amani