Mourinho acharuka tena

47

Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho amevishambulia kwa mara nyingine vyombo vya habari Ijumaa hii, wakati alipoanza kujitetea kwa kirefu kuhusu kumtumia mshambuliaji wa timu ya taifa ya England, Marcus Rashford. Mshambuliaji huyo mwenye miaka 20, alionyesha mchezo mzuri katika michezo ya awali akiwa na kikosi cha Three Lions, katika mechi za mwanzo za michuano ya ligi ya mataifa ya Ulaya, alipofunga katika mechi dhidi ya Uhispania na Uswisi.

Hatua hiyo, imepelekea kuibua maswali mengi ya iwapo Mourinho anautumia ipasavyo uwezo wa Rashford, katika wakati ambapo fowadi huyo anaonekana kupigania nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha United, huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Romelu Lukaku Alexis Sanchez na Anthony Martial. Ni dhahiri kuwa Rashford hataungana na wenzake wakati watakapomenyana na Watford Jumamosi hii, kwa kuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu, baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu, walipomenyana na Burnley, kabla ya kuanza kwa michuano za ligi ya mataifa.

Jose ameeleza kwa kirefu akitoa takwimu zinazoonyesha mechi 105 ambazo Rashford amecheza katika misimu yake miwili ya kwanza akiwa kocha wa timu hiyo. Mourinho amedokeza kuwa wakufunzi wengine wanapaswa kuulizwa namna wanavyowatumia wachezaji chipukizi wa Uingereza.

Amesema, “Marcus Rashford sio Dominic Solanke (mshambuliaji wa Liverpool) na wala sio Ruben Loftus-Cheek (kiungo wa Chelsea), si Dominic Calvert-Lewin (mshambuliaji wa Everton)”. Mourinho amesema yeye ni Marcus Rashford, mchezaji wa Manchester United, ambaye ameonyesha mchezo mzuri wa kiwango cha juu katika mashindano bora zaidi.

Mourinho amekabiliwa na ukosoaji mkali katika wiki chache za mwanzo tangu kuanza kwa msimu wa ligi baada ya kichapo kutoka kwa Brighton na Tottenham, kuifanya timu hiyo kuachwa nyuma zaidi dhidi ya wapinzani wake Liverpool, Chelsea, Spurs na Manchester City. Lakini licha ya kushinda mechi dhidi ya Burnley na kuwa na mapumziko ya wiki mbili ya mechi za kimataifa, Mourinho kwa mara nyingine amewashambulia wanahabari.

“Wale wanaoamka asubuhi na kitu cha kwanza akilini mwao kinakuwa ni Jose Mourinho na Manchester United nawasikitikia sana kwa sababu kuna vitu vingi vingine vya kumfurahisha mtu anapoamka asubuhi, badala ya kuanza kuzungumza kuhusu sisi na kuhusu soka.

Author: Bruce Amani