Mourinho apata kazi Roma Italia wiki mbili tu baada ya kufutwa na Spurs

Kocha wa Kireno Jose Mourinho ameteuliwa kuwa kocha wa AS Roma na ataanza rasmi kukitumikia kikosi hicho mwanzoni mwa msimu ujao 2021/21.

Mourinho mwenye umri wa miaka 58, anachukua mikoba ya Mreno mwezake Paulo Fonseca. Roma mapema Leo Jumanne wametangaza kuwa mwishoni mwa msimu huu Paulo ataachana nao baada ya kuwa na msimu mgumu.

Itakumbukwa Mourinho alifutwa kazi klabuni Tottenham Hotspur Aprili 19 kufuatia matokeo mabovu ndani ya klabu hiyo lakini pia alikuwa anaelekea kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya kwa msimu ujao.

Mourinho amemwaga wino wa miaka mitatu ndani ya timu hiyo ambayo msimu huu iko hatua ya nusu fainali ya Kombe la Europa inacheza na Manchester United.

“Mashabiki bora wamenishawishi kukubali kujiunga na Roma, kwa kweli nahitaji kuanza kazi hata sasa ni nahamu kuwaona”, Alisema Jose Mourinho ambaye kabla ya kujiunga na Spurs amewai kuzinoa klabu za Chelsea, Benfica, Manchester United, Inter Milan na Real Madrid.

“Nashukuru sana familia ya Friedkin kwa kutoa imani kwangu, katika klabu kubwa kama hii. Baada ya kukutana na wamiliki na Tiago Pinto, nimebaini kuwa klabu hii ina mipango mikubwa siku za usoni”, ameongeza.

Mourinho alifutwa kazi baada ya miezi 17 pekee katika klabu ya Spurs, akiwa klabuni hapo timu hiyo ilifungwa mechi 10 kwenye msimu mmoja ikiwa ni mara yake ya kwanza katika taaluma yake.

Anarudi tena Italia baada ya kuhudumu ndani ya Inter Milan na alikuwa sehemu ya historia ya Inter ya kushinda mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Coppa Italia na Serie A mwaka 2009/10.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares