Mourinho asema matatizo yamfanya kutokuwa bora Tottenham

Kocha wa kikosi cha Tottenham Hotspur Jose Mourinho amesema timu yake inakumbwa na matatizo ambayo hawezi kuyatatua mwenyewe ingawa haamini kama Spurs inaweza kuwa kwenye shida kubwa kiasi hicho, ni baada ya Tottenham kupigwa bao 2-1 na West Ham United.

Kinakuwa ni kipigo cha tano katika mechi sita, na sasa kinakamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakati Wagonga Nyundo wa London wakiwa nafasi ya nne.

Michail Antonio na Jesse Lingard walifunga upande wa West Ham wakati Lucas Moura akifunga bao la kufutia machozi.

“Tupo kwenye wakati mgumu, mgumu kwa sababu hatupati matokeo chanya, ni kawaida sehemu yoyote ile, tatizo letu tunapoteza mechi nyingi mno” alisema Mourinho ambaye amewai kuvinoa vilabu kama Manchester United, Chelsea, Real Madrid na Inter Milan.

Mshindi huyo mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa inasemekana kuwa amekalia kuti kavu na kocha wa Leicester City Brendan Rodgers anatajwa kuchukua mikoba yake.

“Nafikiria ndani ya timu hii kuna matatizo ya muda mrefu ambayo siwezi kuyatatua pekee yangu kama kocha” aliongeza.

Bado Mourinho Ana sehemu mbili ambazo zinaweza kumbakiza Spurs au kufanya aondoke. Mosi ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa na pili Kombe la Ligi ambalo yuko fainali na Manchester City.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares