‘Mpango kabambe waandaliwa kuhitimisha ligi ya mabingwa na ligi ya Europa’ – Ceferin

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya Aleksander Cerefin amesema wana mpango kabambe wa kuhakikisha michuano iliyo chini ya Shirikisho hilo inatamatika mwishoni mwa mwezi Agosti.

Mwezi uliopita ilitoka taarifa ya ndani ya taasisi hiyo kuwa ligi ya mabingwa Ulaya na ligi ya Europa zingemalizika mwezi huo (wa nane).

Tofauti na ilivyokuwa ilijadiliwa awali kuwa ili kuhakikisha michezo inamalizika kungechezwa mtanange wa raundi moja pekee, lakini kwa maelezo aliyoyatoa leo Ceferin amesema raundi zote mbili za robo fainali na nusu fainali zitapigwa kama kawaida.

Akizungumza na kituo kimoja cha Habari leo Jumapili kiongozi huyo wa Mpira wa miguu Ulaya amesema “Kwa namna mambo yanavyokwenda hivi sasa, nina uhakika tunaweza kuhitimisha msimu huu salama”.

Cerefin ameongeza kwa kusema “michezo yote itachezwa bila uwepo wa mashabiki”.

VIPI LIGI ZA NDANI?

Ligi Kuu nchini England imebakiza raundi 9 ili kumalizika na tayari utaratibu umekuwa ukifanyika kuhakikisha ligi inachezwa na kumalizika.

Upande wa Ufaransa tayari matajiri Paris Saint Germain wametawazwa kuwa mabingwa watetezi wa taji la Ligue 1 baada ya serikali nchini humo kufuta shughuli za michezo kwa msimu wa 2019/20.

Aidha, ligi ya Ujerumani Bundesliga imerejea rasmi Jumamosi hii ya tarehe 16 Mei ambapo mitanange itakuwa ikipigwa bila uwepo wa mashabiki, wakati ligi ya Hispania La Liga inakusudiwa kurejea mwezi Juni.

Author: Bruce Amani