Mshambuliaji wa Azam Prince Dube aangaza macho yake kwenye kiatu cha dhahabu msimu huu

Mshambuliaji wa kikosi cha Azam FC Prince Dube raia wa Zimbabwe amesema atazidi kupambana kuhakikisha anafikia matamanio ya kuwania kiatu cha ufungaji bora mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21.

Dube ameyasema hayo baada ya kufikisha mabao 12 na kuwa kinara akimzidi bao moja mshambuliaji wa kimataifa wa Simba Meddie Kagere.

Kwa misimu miwili mfululizo, Kagere amefanikiwa kutwaa Tuzo ya Ufungaji Bora katika Ligi Kuu Bara na msimu huu anaifukuzia kwa mara ya tatu.

Kwa sasa Kagere ndani ya Simba ametupia mabao 11 anafuatiwa na John Bocco mwenye mabao 10 kibindoni.

Dube amewashukuru wachezaji wenzake kwa namna ambavyo wamekuwa wakimpa ushirikiano kufikia matamanio na ndoto zake katika msimu huu wa mashindano.

Dube ambaye amejiunga na Azam msimu huu akitokea klabu ya Highlanders FC ya Zimbabwe, alifunga bao la 12 dhidi ya Yanga wikiendi iliyopita.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares