Msimu utafutwa kama mpango A, B na C utafeli – Rais wa Uefa Ceferin


Rais wa Uefa Aleksander Ceferin amesema msimu wa soka utafutwa kama utashindwa kuendelea mpaka mwishoni mwa mwezi Juni.

Ligi mbalimbali Ulaya zimesimamishwa kutokana na janga la virusi vya Corona, ambapo mashindano ya Euro 2020 yaliyotakiwa kufanyika mwaka huu mwezi Juni yamehairishwa pia mpaka 2021.

Ceferin amesema ligi zitaweza kumalizika hata kuchezwa bila uwepo wa mashabiki.

“Kama tutashindwa kumalizia ligi, msimu wa mashindano utakuwa umefutwa,” amesema caferin ambaye ni raia wa Slovenia.

“Tuna mpango A, B, na C, tukishindwa kuanza mwezi Mei,tutaanza Juni tukishindwa hapo tutacheza mwishoni mwa Juni ikishindikana hapo basi huenda tutafuta msimu.”

Wakati michezo inasimamishwa, EPL ilikuwa imebakiza mechi 9 pekee kwa kila klabu, mechi 12 kwa ligi nyingine barani Ulaya.

Aidha, Ceferin aliongeza kwa kusema mechi kuchezwa bila mashabiki itakuwa njia ya mwisho kisha itatumika katika nchi zote zilizo chini ya bara la Ulaya licha ya kukiri michezo kuendelea bila mashabiki haipendezi na haivuti lakini wataangalia njia bora zaidi ya kuhitimisha msimu huu wa mashindano.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends