Mtibwa Sugar kuikabili Northern Dynamo katika CAF

15

Ngoja ngoja sasa imemalizika mara baada ya kusubiri kwa muda mrefu mashindano ya klabu bingwa Afrika na kombe la shirikisho la Afrika CAF sasa mda umewadia.

Ratiba ya michezo ya kombe la Shirikisho imepanga kuanza kuchezwa Jumanne ya wiki hii huku Tanzania bara ikiwakilishwa na Mtibwa Sugar ambayo itashuka katika dimba la Azam Complex kumenyana vikali na Northern Dynamo kutokea kisiwa cha Ushelisheli.

Mchezo huo umepangwa kupigwa majira ya saa kumi kamili jioni kwa masaa ya Afrika Mashariki

Mtibwa Sugar ilipata fursa hiyo baada ya kuibuka kidedea kwenye mashindano ya kombe la FA dhidi ya Singida United.  Hii sio mara ya kwanza kwa vijana wa Zubery Katwila kushiriki mashindano makubwa kwani hata kwenye msimu wa 2003/2004 pia ilishiriki ingawa haikumaliza ratiba yake hivyo kukutana na rungu la CAF.

Kuelekea mchezo huo viingilio vimewekwa bayana ambapo VIP itakuwa Tsh 3000 na sehemu nyingine za uwanja huo ambao unamilikiwa na klabu ya Azam FC itakuwa tsh 2000, hii ni katika kutoa mwitikio wa mashabiki kujitokeza kwa wingi kwa mjibu wa msemaji wa klabu hiyo Tobias Kifaru ‘Ligarambwike’.

Mtibwa Sugar ambayo inashiriki katika TPL ni miongoni mwa timu ambazo haziamini sana katika wachezaji wa kigeni mpaka sasa haina mchezaji yeyote kutoka nje pamoja na Kocha ni mzawa, Zubery Katwila.

Kwa upande wa Northern Dynamo katika ligi daraja la kwanza Sheli Sheli haifanyi vizuri sana kama ilivyokuwa msimu wa 2017 ambapo ulikuwa katika kiwango bora sana.

Mtanange huo utakuwa ni raundi ya kwanza ambapo Mtibwa Sugar italazimika kuifuata Northern Dynamo wiki mbili baada ya mchezo huo kupigwa Azam Complex nje kidogo la jiji la Dar es Salaam.

Author: Bruce Amani