Mwakyembe apania kurudisha ligi kuu ya kandanda Tanzania

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini Tanzania imesema itaanza kurejesha michezo ya ligi za mpira wa miguu kisha watafikiria kuhusiana na michezo mingine.

Hayo yameelezwa na waziri Dkt Harrison Mwakyembe kupitia ukurasa rasmi wa Wizara hiyo ambapo mbali na hivyo ameweka wazi juu ya ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha maendeleo na Michezo Malya.

“Sisi tumekubaliana na wataalam wetu kwamba tufungulie ligi zilizokuwa zinaendelea za Soka tu, michezo mingine isubiri kidogo ili tunavyoendelea vizuri katika kumalizia viporo vya hizi ligi tutajua namna ya kufungulia michezo mingine”.

Kauli ya Waziri Mwakyembe inakuja siku chache baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kusema kama hali ya maambukizi itaendelea kupungua Tanzania kama ilivyotokea wiki za nyuma atarejesha michezo kama kawaida pamoja na vyuo ili watoto waendelea kusoma kama awali.

Takribani mechi 10 zimesalia kwa timu nyingi kuhitimisha msimu wa 2019/20 kwa vilabu vya Ligi Kuu Tanzania Bara hata hivyo bado kuna mchuano wa FA ambao hutumika kumpata balozi wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends