Namungo FC warudi Tanzania baada ya “Figisu” za CD Primeiro de Agosto ya Angola

Kikosi cha Namungo FC kimerejea nyumbani Tanzania leo Jumatatu baada ya kukwama Angola ambapo kilikwenda kwa ajili ya kushiriki mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CD Primeiro de Agosto.

Kikosi hicho kilizuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Luanda, Angola kwa maelezo kwamba kuna wachezaji watatu na kiongozi mmoja wamekutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, jambo ambalo uongozi wanalichukulia kama figisu za soka la Tanzania.

Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu amesema wamenyanyaswa bila sababu za msingi kwa kuwa sababu za kuzuiwa kwao ni za uongo mtupu.

“Tumezuiwa bila sababu na tumenyanywaswa kwa kuwa walitaka tuwaache wenzentu wanne na sehemu ambayo walipelekwa haikuwa salama kwa kuwa hakukuwa na huduma yoyote ambayo wamepewa.

“Wametuambia kwamba walikuwa wamewapima mara mbili ila sisi tulipoongea nao wamesema hawajapimwa tena, katika hili hatuna amani tunahitaji kurudi Tanzania kwa amani, mtuombee Watanzania ili turudi salama,”.

Jana (Jumapili) kilikwama kuanza safari kwa kuwa mamlaka ya Angola ilitaka watu hao wanne waachwe karantini jambo ambalo hawakukubaliana nalo.

Baada ya mambo kukaa sawa leo Februari 15 wanatarajia kurudi Tanzania huku wakisubiri maamuzi ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Afrika,(Caf) kuhusu mchezo huo ambao ulipaswa kuchezwa Februari 14.

Mchezo huo ulifutwa na CAF wenyewe baada ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kufuatilia suala hilo ambalo limekuwa kwenye mazingira ya hujuma kwa kivuli cha Corona.

Wachezaji wake wanne na kiongozi mmoja watabaki karantini nchini Angola kwa kuwa hawajaruhusiwa kutoka na mamlaka ya Angola.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares