Napoli yafukuzana na vinara Juventus

Katika mchezo ambao ulisimamishwa kwa zaidi ya dakika 15 kwa sababu ya mvua, Napoli nusra iyaone matumaini yao ya ubingwa wa Seria A yakiloweshwa pia.

Napoli walipambana kutoka kuwa nyuma na walihitaji bao la kujifunga Genoa katika dakika za mwisho ili kupata ushindi wa 2-1 na kupunguza pengo lao na vinara na Juventus.

Ushindi huo umeisogeza Napoli alama tatu nyuma ya Juventus ambao wana mchezo leo Jumapili dhidi ya AC Milan. Nayo Inter Milan itaweza kukwea nafasi za juu endapo itapata ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Atalanta.

Genoa ni timu pekee iliyochukua alama dhidi ya Juventus katika ligi hiyo ingawa ilipoteza kwa kufungwa 5-0 na Inter Milan wiki iliyopita.

Lorenzo Insigne aligongesha mtambaa wa panya kwa shuti kali kwa upande wa Napoli kabla ya kushitushwa na bao la kuongoza la Genoa lililofungwa na Christian Koume kwa njia ya kichwa baada ya krosi murua katika dakika ya 20 ya mchezo huo.

Kulikuwa na mvua kubwa mjini Genoa na mchezo ukasimamishwa katika dakika ya 59 kwa karibu dakika 13 hadi mvua ilipoacha kumwagika na uwanja kupunguzwa maji.

Napoli ilisawazisha mapema kabisa baada ya mchezo kuanza, kutokana na wachezaji wawili wa akiba walioingia ambao waliamsha ari mpya kwenye kikosi hicho. Walikuwa ni Martens ambaye alitengeneza goli kwa Fabian Ruiz.

Napoli iliumaliza mchezo huo baada ya mlinzi wa Genoa Davide Biraschi kuugusa mpira uliopigwa na Mario Rui ambapo ulienda kutinga wavuni.

Michezo mingine

Cagliari ilitoka nyuma goli mbili kwa bila dhidi ya Spal na kulazimisha sare ya  2-2 huku wakifunga magoli mawili ndani ya dakika tatu.

Nalo goli la mapema la Gervinho na Roberto Inglese yaliisaidia Parma kumaliza michezo 6 bila kufungwa baada ya jana Torino kukubali kipigo cha 2-1.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends