Nasreddine tambo kibao Yanga

Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi Mohamed amesema anahitaji kuvuna alama sita katika michezo miwili ya ugenini kabla ya kuivaa Simba katika mchezo wa tatu wa Ligi Kuu utakaopigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam ambapo Young Africans watakuwa wenyeji.

Nabi ambaye alikuwa Sudan kabla ya kuja Tanzania, amesema kabla ya kupata alama hizo sita ni lazima kikosi chake kicheza kwa juhudi huku wakiwa na tahadhari ya majeruhi kufuatia Yacouba Sogne kuumia.

Kwenye mechi hizo mbili za ugenini, mabingwa wa kihistoria Yanga itaanza kucheza Jumamosi ambapo itapepetana na Namungo Fc mtanange utakaopigwa dimba la Ilulu kabla ya kukwaruzana na Mbeya Kwanza mchezo utakaopigwa dimba la Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya.

Baada ya hapo itakuwa Kariakooo Derby ambapo utakuwa mchezo wa 107 baina ya timu hizo mbili kwenye mbilinge mbilinge za Ligi Kuu pekee.

“Kutakuwa na mabadiliko ya kikosi hilo ni uhakika tunatakiwa kuwa kamilifu zaidi katika mechi hizo, tukianzia na hii ya Namungo tayari nimezungumza na wachezaji watakaopata nafasi kupambana kwa nia ya kuendeleza rekodi nzuri ya timu,” alisema Nabi na kuongeza;

“Tunatakiwa kuwa makini kila mchezo, kwani ni kama fainali, nimewaambia wachezaji hakuna mechi rahisi tunatakiwa kushinda kwa ubora wa mbinu zetu. Tunatakiwa kumaliza mechi hizo za mkoani, kisha tujipange dhidi ya Simba.”

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends