Natarajia kumuona Messi akimalizia soka lake Barcelona – Pep Guardiola

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema angependelea kumuona staa wa miamba ya soka Uhispania na Argentina Lionel Messi akimalizia soka la ushindani katika klabu ya Barcelona licha ya kuhusishwa kutua ndani ya City.

Guardiola ambaye ameingia kandarasi mpya ya miaka miwili ndani ya matajiri hao wa Jiji la Manchester siku ya Alhamis, siku za usoni amekuwa akihusishwa kutua Barcelona na taarifa nyingine zikisema kuwa wanataka kuungana.

Mkataba wa Messi unamalizika mwishoni mwa msimu huu na inatajwa kuwa Manchester City na Paris St-Germain zitakuwa kwenye nafasi za kutuma ofa zao. Guardiola alisema: “Messi ni mchezaji wa Barcelona. Nimelisema hilo zaidi ya mara elfu moja sasa. Kama shabiki wa Barcelona, mshabiki wa Messi ningependa kumuona anasalia pale”.

Author: Bruce Amani