Neville amkosoa Solskjaer wa Man United

Mchambuzi wa kandanda barani Ulaya Gary Neville amesema kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer lazima aongeze juhudi na kuweza kushinda mataji baada ya usajili mkubwa wa Cristiano Ronaldo na Jadon Sancho.

Kocha huyo raia wa Norwei na mchezaji wa zamani wa Man United aliichukua timu hiyo mwaka 2018 kutoka mikononi mwa Jose Mourinho, ambapo imekuwa ikisemwa kuwa endapo atashindwa kutwaa ubingwa wowote msimu huu anaweza kufurushwa.

Usajili wa Raphael Varane, Jadon Sancho na Ronaldo unaonekana kuongeza presha kwa kocha Solskjaer jambo ambalo linampa nguvu Gary Neville kusema kuwa lazima aboreshe mbinu zake.

‘Kama Ole angekuwa kocha baada ya kuondoka tu kwa Sir Alex Ferguson United basi Ole angefutwa kazi muda mrefu” alisema.

‘Wanashindwa kumuondoa kutokana na makocha wengi kuondoka kwa muda mfupi miaka miwili mitatu au miezi”.

“Ukiwa na Ronaldo lazima ushinde mataji na sio kushika nafasi ya pili, tatu au nne badala yake ni ubingwa, jambo la pili Solskjaer lazima aboreshe kiwango”, ni mambo mawili ambayo Neville anataka kuyaona Manchester United.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends