N’Golo Kante, Chilwell wampasua kichwa Tuchel Chelsea

Kiungo mkabaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa N’Golo Kante na beki wa kushoto wa Chelsea Ben Chilwell wanategemewa kufanyiwa uchunguzi leo Jumatano wa kubaini ukubwa wa majeruhi waliyoyapata kwenye mechi ya ushindi wa goli 4-0 dhidi ya Juventus mtanange uliopigwa dimba la Stamford Bridge Jumanne.

Wawili hao kwa nyakati tofauti walitolewa uwanjani kwa lazima kutokana na kupata maumivu, Chilwell alitolewa ungwe ya pili kunako dakika ya 71 lakini Kante alitolewa muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko.

Hofu kwa Chelsea ni kuwa wachezaji hao wanaumia kipindi ambacho timu hiyo inajiandaa kucheza mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United Jumapili saa 12:30 jioni.

Akizungumzia majeruhi hayo kocha wa Chelsea Thomas Tuchel amesema kuwa Ben Chilwell anaonekana kuwa na maumivu kwenye goti lake wakati N’Golo Kante kiungo wa zamani wa Leicester City pia akionekana kuugulia maumivu kidogo.

“Ni bahati mbaya kwao wote maana walikuwa kwenye ubora mkubwa kwenye mechi ya leo(jana)” alisema

Kocha Tuchel ambaye ameshinda m chi 35 kati ya 50 The Blues, aliongeza kuwa “Ben alionekana kuumia sana lakini kwa sasa anaendelea vizuri”.

Kwenye mchezo wa Uefa, magoli ya Chelsea yamefungwa na beki, Trevoh Chalobah, Reece James, Callum Hudson-Odoi na Timo Werner, ushindi ambao unawapa uhakika wa kucheza 16 bora kukiwa na mchezo mmoja mkononi.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends