Ngoma ya Mkude Simba yalala, Kamati yatoa sababu

Kamati ya nidhamu ya klabu ya Simba imeshindwa kufikia hitimisho la maamuzi juu ya makosa mawili ambayo kiungo mkabaji Jonas Gerrard Mkude anakabiliwa nayo ikiwa ni pamoja na kutoripoti kambini na kushindwa kufanya mazoezi tarehe 18/5/2021.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Suleiman Kova baada ya kuketi sJumatatu na kusikiliza utetezi wa pande zote mbili huku Mkude akiwakilishwa na Wakili Msomi Tumaini Mfinanga imeona ni vyema mchezaji huyo akafanyiwe vipimo vya afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya maamuzi kuchukuliwa.

Kamati hiyo imesema imeona ni busara kujali afya kwanza ya mchezaji kabla ya kutoa maamuzi yake, pia imebaini makosa yaliyojitokeza awamu hii yamekuwa mwendelezo kwa mchezaji huyo kutuhumiwa nayo, hivyo baada ya kupokea ripoti ya kitabibu Kamati itakutana tena na kutoa maamuzi yake.

Kwa sasa Jonas Gerrard Mkude yuko nje ya timu, huku taarifa za awali zikieleza kuwa mchezaji huyo amepigwa ‘stop’ kucheza klabuni hapo mpaka hukumu itakapotolewa.

Wakati hayo yakijili inaelezwa pia kuwa mkataba wa mchezaji huyo unaelekea ukingoni na klabu kubwa nchini zimekuwa zikimnyemelea nyota huyo aliyepoteza namba katika kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares