Ni vigumu kuendeleza kiwango cha msimu uliopita – kocha wa Bayern Munich Flick

96

Ikiwa pazia la Ligi ya Mabingwa Ulaya linafunguliwa rasmi leo kwa Mabingwa watetezi wa taji hilo Bayern Munich kocha wa kikosi hicho Hansi Flick anasema ni vigumu kubakia katika kiwango cha juu kama msimu uliopita.

Bayern Munich watakuwa kwenye kibarua kizito cha kuikabili timu yenye ushindani mkubwa Atletico Madrid katika mtanange wa kundi A.

Bayern walilazimika kupunguza siku za maandalizi ya msimu mpya baada ya kuwa na siku takribani 26 tangia walipocheza mechi ya fainali ya Ligi mabingwa dhidi ya Paris St-Germain na tarehe ya mchezo wa ufunguzi ya Bundesliga.

Bayern walishinda pia taji la Ligi Kuu nchini Ujerumani na Kombe la Ligi na kushinda jumla ya mataji matatu (treble) ingawa majina makubwa baadhi yao yameondoka kama vile Thiago Alcantara na Phillipe Coutinho.

“Itakuwa vigumu kuwa tulivyokuwa msimu uliopita, kila timu imeimarika zaidi msimu huu licha ya mapungufu ambayo huwa hayakosekani kwenye timu” alisema Flick ambaye atacheza mechi ya kwanza Uefa bila uwepo wa majeruhi Leroy Sane na Tanguy Nianzou.

“Tulikuwa na wiki moja pekee ya maandalizi, lakini hivi sasa angalau nimeridhika, wiki moja haitoshi lakini nafurahia kwa sababu sina majeruhi wengi” aliongeza Kocha huyo.

Atletico watakuwa na matumaini ya kufuta uteja na vilabu kutokea Ujerumani baada ya msimu uliopita kupoteza kwa RB Leipzig hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, hasa ikichagizwa na uwepo wa ingizo jipya ambalo ni mshambuliaji wa Uruguy Luis Suárez.

Author: Asifiwe Mbembela