Nigeria Yaondoshwa na Ghana Kufuzu Kombe la Dunia

99

Licha ya kupigiwa chapuo. Licha ya kuwa na vipaji vingi. Licha ya Ghana kutokuwa na wakati mzuri, licha ya kucheza uwanja wa nyumbani, Nigeria imekosa nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia Qatar 2022 baada ya kuondolewa kwa faida ya goli la ugenini.

Pengine mwenye bahati habahatishi. Ndiyo. Super Eagles wa Nigeria wakiwa katika dimba lao la nyumbani la Abuja wamejikuta wakilazimishwa sare ya goli 1-1 katika mchezo wa mkondo wa pili baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa sare tasa na hivyo Ghana ambayo kwa sasa haina ubora ule kusonga mbele kuelekea Qatar baadaye mwaka huu.

Nigeria ikiwa moja ya taifa ambalo limesheheni vipaji lukuki kama vile Joe Aribo, Emmanuel Dennis, Lookman, Daniel Amartey, Kelechi Ihenancho, Ighalo bado wameshindwa kuifungua safu imara na mbinu za kocha wa Ghana Otto Addo kwa dakika zote 90.

Kwenye mechi hiyo, Thomas Partey alifunga bao kabla ya beki wa Watford Trost-Ekong kufunga goli kwa njia ya penati baada ya winga wa Leicester City Ademola Lookman kufanyiwa faulo.

Author: Asifiwe Mbembela