Nigeria yawatupa nje mabingwa watetezi

147
Hatimaye bingwa mpya wa kombe la Mataifa Afrika Afcon 2019 ndani ya ardhi ya Misri atapatikana baada ya bingwa mtetezi Cameroon kufungashiwa mizigo yake leo Jumamosi Julai 7.
Cameroon akiwa bingwa mtetezi amejikuta akipoteza sifa hiyo mbele ya wababe Nigeria waliofanikiwa kushinda goli 3-2 katika mchezo uliokuwa wa kupokezana katika kumiliki na kushambuliana hatua ya 16 bora.
Goli za Cameroon zimefungwa na Stephane Bahoken na Clinton Njie baada ya goli la mapema la Odion Ighalo na matokeo kuwa 2-1 kwenda mapumziko kabla ya Ighalo kusawazisha kipindi cha pili na winga wa Arsenal Alex Iwobi kufunga goli la ushindi.
Licha ya kuongoza mechi kwa kupata goli la mapema vijana wa Super Eagles waliduwaa na kujikuta Cameroon ikiongoza mechi 2-1 kwenye kipindi cha pili kabla ya vijana wa Nigeria kupindua matokeo mpaka mwisho 3-2.
Kocha Gernot Rohr alipata shutuma nyingi kwenye mechi za makundi kutokana na kiwango duni huku kupoteza dhidi ya Madagascar ikiwa changamoto kubwa zaidi, matokeo ya leo yatakuwa yamerejesha amani ndani ya kikosi cha Super Eagles hao. Robo fainali ni Nigeria vs Afrika Kusini.

Author: Asifiwe Mbembela