Niyonzima awaliza mashabiki Yanga, Ihefu waomba “Poo”

Pengine usemi wa kitu hakionekani kuwa na thamani mpaka kitoweke ndiyo imedhihirika katika kandanda ya Yanga na Ihefu baada ya dakika 90 kukamilika na Haruna Hakizimana Niyonzima kuchukua kipaza sauti na kusema viongozi kwakherini, wadau kwakherini, na mashabiki kwakherini.

Kutaja tu neno mashabiki, baadhi yao mwenye roho nyepesi walijikuta “automatic” machozi yakiwalenga na kuwatoka wakiwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Machozi hayo, yanaweza kuwa na picha mbili; kwanza si ajabu wanaolia ndiyo waliochoma jezi yake, kipindi kile Niyonzima anakatisha mtaa kutoka Jangwani kwenda Msimbazi Kariakoo kujiunga na Simba, waliomuona kama msaliti.
Lakini kama haitoshi, pengine ni machozi ya mwisho ya ubaya aibu.
Hata hivyo, ukiweka skendo hiyo ambayo iliwaumiza Wanayanga ya kwenda Simba,  Niyonzima katika miaka saba na nusu ndani ya Timu ya Wananchi aliitumikia kwa moyo wote, akiteka na kuwakonga mashabiki wa timu hiyo, pia alikuwa sehemu ya kikosi kilichobeba ubingwa mara tatu mfululizo “Kampa Kampa Tena”. Machozi hawana budi kuyatoa.
Niyonzima ameondoka Yanga kwa ushindi wa mabao 2-0 na kusepa na pointi hizo katika mchezo ambao kiungo mshambuliaji Feisal Salum Fei Toto akifunga magoli yote mawili yakiwa yanatoa neno la kwa kheri kwa “Baba Mzazi Baba” wa Kisenyi.
Jitihada za Ihefu kuweza kuweka usawa mzani ziligonga mwamba na kufanya timu hiyo kupoteza jumla ya Pointi sita mbele ya Yanga.
Mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0 Uwanja wa Sokoine na leo imepoteza kwa kufungwa mabao 2-0 Uwanja wa Mkapa.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares