Niyonzima kuagwa Yanga mbele ya mashabiki, Ihefu hofu lukuki

Kikosi cha Yanga kimetamba kuendeleza moto wa ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu huku mechi hiyo ikitumika kumuuga kiungo Maestro Haruna Hakizimana Niyonzima aliyeitumikia klabu hiyo kwa takribani miaka saba.

Yanga inaingia kwenye mechi ya Leo Alhamis Julai 15 ikijua kuwa alama moja katika mechi mbili zilizosalia zitaifanya kumaliza nafasi ya pili na kuwazidi kete wapinzani wao wa karibu katika nafasi hiyo klabu ya Azam FC.
Mtanange huo utapigwa dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam majira ya saa 10 jioni huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Desemba 23, mwaka jana.
Akizungumzia maandalizi yao, Ofisa habari wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli amesema: “Maandalizi yetu hayalengi timu moja pekee, bali tunajua ratiba yetu ina michezo miwili iliyosalia kwenye Ligi Kuu Bara, ambayo ni dhidi ya Ihefu, na Dodoma Jiji. Malengo yetu ni kushinda michezo hiyo ili kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo.”
Ihefu wanahitaji alama tatu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusalia VPL.
Mnyarwanda Niyonzima anategemewa kuagwa leo baada ya makubaliano baina ya pande mbili. Mbali na mchezo huo, michezo mingine leo ni pamoja na Azam Vs Simba, Tanzania Prisons Vs Biashara United, Mbeya City Vs Gwambina, Dodoma Jiji Vs Mtibwa Sugar na nyinginezo.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares