Nyota wa mpira wa kikapu afariki dunia katika ajali ya helikopta

Ulimwengu wa michezo unaomboleza kifo cha nguli wa mpira wa kikapu nchini Marekani. Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amekuwa miongoni mwa watu wa awali mashuhuri waliotuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha nyota wa zamani wa mpira wa kikapu wa timu ya LA Lakers Kobe Bryant aliyefariki dunia Jumapili kwenye ajali ya helikopta. Obama ameungana na wachezaji wengine nyota wa zamani wa mchezo huo kuelezea hisia zao baada ya kifo hicho ambao ni pamoja na Shaquille O’Neill, Magic Johnson, Michael Jordan na Kareem Abdul – Jabar. Bryant amefariki dunia pamoja na binti yake wa miaka 13 Gianna, pamoja na watu wengine saba waliokuwa kwenye helikopta hiyo iliyoanguka kwenye eneo la Calabasas, jijini Los Angeles. Mkuu wa polisi jijini Los Angeles Alex Villanueva hata hivyo hakuwatambulisha watu hao wengine, akisema wanasubiri uchunguzi wa miili utakapokamilika.

Author: Bruce Amani