Origi aizamisha Everton katika dakika ya mwisho

Mchezaji ambaye wengi walikuwa wamesahau kuwa bado yuko katika klabu ya Liverpool, ndiye aliyefunga bao la pekee na la ushindi ambalo liliipa Liverpool fursa ya kujigamba mbele ya watani wao wa Merseyside Everton. Divock Origi alifunga bao la kushangaza la dakika ya 96 baada ya kosa la kipa Jordan Pickford kuizawadia Liverpool ushindi uwanjani Anfield.

Lilimfanya kocha Jurgen Klopp kukimbia hadi uwanjani kwenda kumkumbatia kipa Alisson na mashabiki wakanyanyuka kwa shangwe huku Everton wasiamiamini macho yao baada ya kufanya kazi kubwa sana uwanjani.

Mchuano huo wa 232 kati ya mahasimu hao wa mjini ulionekana kukamilika kwa sare wakati Pickford aliutema mpira uliopitwa na Virgil van Dijk na ukamwagukia Origi baada ya kugonga besela. Origi akafunga kwa kichwa. Liverpool sasa wamejiimarisha katika nafasi ya pili, pointi mbili nyuma ya vinara na mabingwa watetezi Manchester City.

Everton wanabaki bila ya ushindi katika mechi zao 18 za mwisho dhidi ya Liverpool na hawajapata ushindi uwanjani Anfield katika karne hii.

Wako katika nafasi ya sita, pointi nane nyuma ya Tottenham katika nafasi ya tano na Arsenal ya nne.

Aubameyang alikuwa moto wa kuotea mbali

Arsenal majogoo wa London

Awali, Arsenal walionyesha mchezo wa hali ya juu na kuwanyamazisha mahasimu wao wa London, Tottenham Hotspur katika mtanange mkali na wa kusisimua uliochezwa uwanjani Emirates

Vijana hao wa Unai Emery waliwafunga Spurs 4-2 na kufikisha mechi 19 mfuulizo bila kushindwa. Wamesonga mbele ya Spurs katika nafasi ya nne.

Arsenal walitangulia kufunga kupitia penalti ya Pierre-Emerick Aubameyang baada ya Jan Vertonghen kuunawa mpira

Spurs walisawazisha kabla ya kipindi cha mapumziko kupitia bao la kichwa lake Eric Dier kutokana na mkwaju wa freekick. Harry Kane alifunga la pili baada ya rob Holding kusemekana kumwangusha kwenye kijisanduku Son Heung-min

Kipindi cha pili Emery alimleta Alexandre Lacazette na Aaron Ramsey. Ramsey akampa pasi safi Aubameyang akasawazisha. Lacazette akafunga la tatu kabla ya Lucas Torreira kufunga kazi.

Chelsea yaibwaga Fulham

Uwanjani Stamford Bridge, mabao ya kila kipindi kutoka kwa Pedro na Ruben Loftus-Cheek yaliipa Chelsea ushindi wa 2-0 dhidi ya mahasimu wao wa kusini magharibi mwa London Fulham.

Ushindi huo umeiweka Chelsea katika nafasi ya tatu, pointi tano nyuma ya Liverpool na moja mbele ya Arsenal ambao wana 30

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends