Otkay ajiuzulu kama kocha wa mabingwa wa Kenya Gor Mahia

Hassan Oktay amejiuzulu rasmi kama kocha wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya – KPL Gor Mahia. Kocha huyo wa Kituruki ameiomba klabu hiyo kumruhusu aachie majukumu yake baada ya kuomba likizo ya siku tano wiki iliyopita.

Otkay aliteuliwa kuwa kocha wa Gor Mahia Desemba 2018 kuchukua nafasi ya Dylan Kerr, ambaye pia alijiuzulu kutoka wadhifa wake baada ya kuwa usukani kwa msimu mmoja tu.

Katika barua yake, Otkay amesema amelazimika kujiuzulu kutokana na changamoto za kifamilia Ulaya.

Klabu ya Gor Mahia imethibitisha kukubali ombi hilo la kujiuzulu kocha Otkay. Kuna ripoti kuwa kocha wa zamani wa klabu za Berekum Chelsea na Asante Kotoko Steven Polack yuko njiani kuchukua mikoba ya Otkay.

Awali, Mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier alifichua kuwa kocha Otkay aliondoka Kenya pamoja na virago vyake wakati kukiwa na ripoti kuwa kocha huyo huenda asirejee tena kwa mabingwa hao wa Kenya.

Otkay aliondoka Kenya Jumatano iliyopita kwenda kushugulikia masuala ya kifamilia nchini Uturuki, na alitarajiwa kurejea nchini Jumanne asubuhi kujiandaa kwa ajili ya mchuano wa CAF Champions League dhidi ya Aigle Noir ya Burundi

“Likizo yake ilikamilika Jumatatu na tulitarajia arejee kazini leo Jumanne. Hajarejea na tuna wasiwasi. Nilitembelea nyumbani kwake na kwa mshangao, alibeba mali zake zote. Alisema Rachier.

Amesema sasa wanasubiri mawasiliano rasmi kutoka kwa kocha huyo kabla ya kutoa tamko lolote kama klabu. “Tuna makocha kadhaa tuliozungumza nao tayari katika siku za nyuma na kama hataonekana tutaijaza nafasi yake, tuko tayari kwa lolote.” Amesema Rachier.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends