Paris St-Germain yachapwa na Monaco licha ya kuendelea kuongoza Ligue 1

Monaco wakitoka nyuma kwa goli mbili dhidi ya Paris St-Germain wamefanikiwa kuibuka kidedea kwa goki 3-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu nchini Ufaransa maarufu kama Ligue 1 wakifuta rekodi ya kushinda mechi nane mfululizo ya matajiri hao.

Matajiri hao wa Jiji la Paris walitangulia kujipatia magoli mawili ya kipindi cha kwanza kupitia kwa Kylian Mbappe ambaye alikuwa anacheza mechi yake ya kwanza kutokea kwenye majeruhi.

Lakini ungwe ya pili ilikuwa ya Monaco ambayo ilibadilika kabisa na kufanikiwa kufunga magoli mawili ya Kevin Volland ndani ya muda mfupi.

Staa wa zamani wa Arsenal na Barcelona Cesc Fabregas alihitimisha furaha ya Monaco kwa kuwaptia bao la penati zikiwa zimesalia dakika sita kumalizika kwa mchezo huo.

Hata hivyo, matokeo hayo hayajabadilisha chochote kwa PSG ambao wanaendelea kuongoza msimamo wa Ligue 1 wakati kwa Monaco yamewasogea katika nafasi nzuri.

Author: Bruce Amani