Pep: Mafanikio ya Man City nyumbani hayana upinzani

310

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema mafanikio ya karibuni ya Manchester City katika kandanda la Uingereza hayana upinzani, baada ya kubeba Kombe la Carabao.

Mabao kutoka kwa Sergio Aguero na Rodri yaliisaidia City kuifunga Aston Villa 2 -1 uwanjani Wembley. Mtanzania Mbwana Samatta aliifungia Villa bao safi la kichwa.

Kando na mataji matatu ya League Cup, Guardiola ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Premier, Kombe la FA na mataji mawili ya Ngao ya Jamii.

“Tangu tulipoanza kushinda, mashindano tisa ya mwisho ya nyumbani tuliyocheza, tumeshinda nane.” amesema Pep. “Hiyo ni safi sana. Hakuna klabu katika historia ya mataji ya Uingereza, bila kuhesabu Ulaya, imeshinda idadi ya mataji tuliyoshinda mfululizo.

Liverpool ilishinda mataji sita ya ligi, mawili ya FA na manne ya League Cup katika miaka 80, wakati Man United ilikusanya mataji 13 ya Ligi ya Premier yakiwemo matatu mfululizo mara mbili chini ya kocha Alex Ferguson, na Arsene Wenger akashinda taji la ligi bila kupoteza mechi hata moja ya msimu.

Author: Bruce Amani