Pesa yamvuta Wijnaldum kutua Paris St-Germain na kuikacha Barcelona

Kiungo mkabaji wa Liverpool na Uholanzi Georginio Wijnaldum amekamilisha uhamisho wa kujiunga na miamba ya soka la Ufaransa Paris St-Germain akitokea Liverpool kama mchezaji huru.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30, aliamua kutoongeza mkataba mpya wa kuendelea kukitumikia kikosi cha Liverpool na kujiunga na PSG licha ya kuwa awali alikuwa anahusishwa kujiunga na Fc Barcelona.
“Najiunga na moja ya timu kubwa barani Ulaya, nitaweka juhudi zangu zote kuhakikisha nasaidia katika mpango wao” alisema Wijnaldum.
Wijnaldum alijiunga na Liverpool kutokea Newcastle United mwaka 2016 kwa ada ya pauni milioni 25.
Imefahamika kuwa PSG walituma ofa nzuri zaidi ya ile ya Barcelona ingawa uwepo wa kocha Mauricio Pochettino ndani ya klabu hiyo ni sababu nyingine ya mchezaji huyo kwenda Parc Des Princes.
Kwa sasa Wijnaldum anajiandaa na michuano ya Euro 2020 inayoanza kutimua vumbi Ijumaa ya Juni 11 ambapo yupo na kikosi cha Uholanzi.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares