Pochettino ahusishwa Man United

Kocha wa kikosi cha matajiri wa Jiji la Paris, Paris St-Germain Mauricio Pochettino ameweka wazi kuwa anaweza kuondoka klabuni hapo endapo ofa na mpango mzuri utawekwa na klabu ya Manchester United ili kurithi mikoba ya Ole Gunnar Solskjaer aliyetimuliwa Jumapili.

Kocha huyo raia wa Argentine mwenye umri wa miaka 49, amekuwa akihusishwa kurudi England mara kadhaa ambapo kwa sasa nafasi ya kufundisha Mashetani Wekundu inaonekana kuwa fursa yake adhimu hasa kutokana na kuwa na kipindi kigumu Ufaransa.

Muda mzuri wa takribani miaka mitano Tottenham Hotspur umekuwa kivutio kikubwa kwa Pochettino kumfanya atamani tena kurejea kufundisha soka katika klabu moja wapo England.

Bado hakuna ofa yoyote ile ambayo imetumwa kwake lakini ugumu wa kumpata Zinedine Zidane unaweza ukalazimisha upande mwingine kufanikiwa, lakini pia Antonio Conte kuchukuliwa Spurs kunaongeza hali ya wawili hao.

Kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Manchester United na Villarreal mtanange utakaopigwa Hispania Jumanne Novemba 23, Man United imesema timu hiyo itaongozwa na Michael Carrick kama kocha wa muda na kiungo mkabaji wa zamani wa timu.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends