Pointi tatu kwa Man City kuwa mabingwa wa EPL

Vinara wa Ligi Kuu nchini England Manchester City wanaweza kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu siku ya Jumapili, baada ya kuibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Crystal Palace.

City wanaweza kubeba taji la EPL bila kucheza mechi endapo wapinzani wao waliopo nafasi ya pili Man United watapigwa na Liverpool Jumapili.

Magoli ya City yalifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina Sergio Kun Aguero ambaye alianza mchezo wa kwanza kwa takribani mwezi na goli la pili kufungwa na Ferran Torres.

Kwenye ungwe ya kwanza, kikosi cha kocha Roy Hodgson kilipata nafasi ya kukwamisha mpira nyavuni kupitia kwa Christian Benteke ambaye mpira wake uliookolewa na Ederson.

“Hatutakiwi kujiona kama washindi, tunahitaji kushinda mechi zetu” alisema kocha Pep Guardiola baada ya mechi hiyo katika dimba la Crystal Palace.

Alama mbili kwenye mechi zilizosalia zitawapa ubingwa Manchester City ambao Jumanne watacheza dhidi ya Paris St-Germain mchezo wa mkondo wa pili, walishinda bao 2-1 katika dimba Parc Des Princes mkondo wa kwanza.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares