Polisi Tanzania yatota mbele ya Wekundu wa Msimbazi Simba

Simba imeibuka kidedea mbele ya Polisi Tanzania ya Moshi kwa goli 2-1 katika mtanange wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania bara uliopigwa dimba la Taifa leo Jumanne.

Simba waliokuwa wenyeji wa mchezo huo asilimia kubwa ya kikosi kilichoanza kilikuwa tofauti na kile kilichopata matokeo chanya dhidi ya Namungo FC. Kilionekana kulemewa eneo la kiungo na kuruhusu mianya mingi ya kushambuliwa.

Baada ya piga ni kupige, walikuwa ni Polisi Tanzania walioanza kufunga bao la kuongoza lililofungwa kipindi cha kwanza Sixtus Sabilo dakika ya 22 akiwazidi ujanja walinzi wa Simba, Shamte Ally na Tairon Santos.
Tamati ya ngwe ya kwanza bado kinara alikuwa Polisi Tanzania kwa goli 1-0 iliyokuwa kwenye kiwango kizuri katika mchezo wa leo.
Ngwe ya pili ya mwamuzi Hasi Mabena ilikuwa nzuri kwa Simba ambao walipata auheni kupitia goli la nahodha wao John Bocco dakika ya 56 akimalizia pasi ya Clatous Chama.
Wakati mchezo ukiwa katika muda wa nyongeza za mwamuzi wa mezani na kuonekana kama sare, Ibrahim Ajibu alifunga bao la ushindi dakika ya 90 + 5 akimalizia pasi ya Francis Kahata.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 50 huku ikimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa kinara wa ligi hiyo wakati Polisi Tanzania wakibakiwa na pointi 30 katika nafasi ya 7 michezo 19.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments