PSG yaendeleza presha kwa Lille, yaichapa Lens na kwenda kileleni kwa muda mfupi

Matajiri Paris St-Germain wamepata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Lens katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa huku Neymar akiingia kambani mara moja na kutengeneza bao moja.

Ushindi wa PSG unaifanya kuendelea kuipa hofu kinara wa Ligi hiyo Lille ambao watakuwa na mchezo kwa siku ya leo Jumapili.

Nyota wa Kibrazil Neymar Jr alifunga goli la kwanza katika dimba la Parc Des Princes kisha anapiga kona iliyounganishwa na beki Marquinhos.

Lens ambao wanakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligue 1 walipata nafasi ya kukwamisha mpira nyavuni na Ignatius Ganago akakwamisha mpira huo.

Hata hivyo, PSG walifanikiwa kushinda mechi hiyo na kukwea kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya alama mbili na Lille.

Baada ya mchezo wa leo, PSG wanaelekea England kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City mchezo wa nusu fainali mkondo wa pili.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares