PSG yaendeleza rekodi yake kileleni bila huduma za Neymar

Paris St-Germain waliendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi yoyote tangu mwanzo wa msimu baada ya kuwanyeshea Rennes 4 – 1. Timu hiyo ya Kocha Thomas Tuchel imepoteza mechi nne tu katika ligi kutoka kwenye mechi zao 20 za kwanza na wanaongoza msimamo wa Ligue 1 na mwanya wa pointi 13.

Mshambuliaji wa Uruguay Edinson Cavani alifunga bao moja katika kila kipindi cha mchezo, huku mabao mengine yakitiwa kimiani na Angel di Maria na Kylian Mbappe.

Mbaye Niang alikuwa aliwafungia wageni Rennes bao la kufutia machozi lakini PSG walipata ushindi huo rahisi licha ya kukosa huduma za mshambuliaji nyota Mbrazil Neymar. Neymar anaweza kukosa mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 ya Champions League dhidi ya Manchester United Jumanne Februari 12. Kocha Tuchel alisema “Itakuwa vigumu sana. Ni mapema sana kuzungumzia tarehe ya kurejea kwake kwa sababu tunapaswa kusubiri na kuona atakavyoendelea kupewa matibabu na lazima tuwe na uhakika na hilo.”

Author: Bruce Amani