Putin ailaani hatua ya WADA kuifungia Urusi

Rais wa Urusi Vladimir Putin, amelaani hatua ya Shirika la dunia linalopambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini kwa wanamichezo WADA, kwa kuifungia nchi yake kutoshiriki katika mashindano ya kimataifa kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Hatua hii ya WADA, inamaanisha kuwa, Urusi haitashiriki katika michezo ya Olimpiki mwaka 2020, itakayofanyika jijini Tokyo nchini Japan lakini pia kombe la dunia nchini Qatar mwaka 2022.

Hatua hii imekuja, baada ya maafisa wa WADA kukutana jijini Lausanne, nchini Uswisi baada ya kuishtumu serikali ya Urusi kwa kufanya udanganyifu kuhusu matokeo ya vipimo vya wanamichezo waliofanyiwa ucbunguzi mapema mwaka huu.

Adhabu hii pia inawazuia viongozi wa serikali kutoshiriki katika matukio makubwa ya michezo, lakini pia Urusi haitaweza kuwa mwenyeji wa ma mashindano mbalimbali ya Kimataifa.

Rais wa WADA, Craig Reedie amesema kuwa Urusi ilipewa fursa ya kipekee ya kujisafisha ili kurejea tena katika ulimwengu wa michezo, lakini imeendelea kukanusha kuwasaidia wanamichezo wake hasa wanariadha kutumia dawa za kuwaongezea nguvu mwilini.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends