Rais Magufuli atafakari kurudisha michezo Tanzania

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amesema idadi ya wagonjwa wa Virusi vya Corona katika vituo vilivyotengwa imepungua sana, hivyo anaangalia wiki inayoanza kesho, kama hali itaendelea kuwa hivi, ataamua kufungua vyuo na kuruhusu michezo iendelee.

JPM amesema michezo ni sehemu ya burudani kwa Watanzania hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuangalia uwezekano wa kurejesha michezo nchini.

Rais Magufuli amezungumza hayo leo Jumapili katika kanisa la KKKT, ushirika wa Chato, Mkoani Geita, ambako ndiko ameweka makazi katika kipindi hiki.

Machi 17, 2020 Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu ilizuia mikusanyiko isiyo ya lazima kutokana na janga la Virusi vya Corona ambalo lililoitikisa Dunia.

Kauli ya leo ya Rais Magufuli inakuwa ya pili kuhusiana na kurejesha michezo nchini kwani mwezi huu mwanzoni wakati akimwapisha Mwingulu Nchemba katika Wizara ya Katiba na Sheria alisema anafikiria kurudisha michezo.

Author: Bruce Amani