Rais wa Caf afika Tanzania, ateta na Waziri Mkuu Majaliwa

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekutana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe Dodoma na kujadiliana na masuala kadhaa ya maendeleo ya mpira wa miguu.

Katika Taarifa iliyotolewa na CAF, kikao hicho kimefanyika muda mfupi baada ya Motsepe kuwasili Leo nchini ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa Rais wa shirikisho hilo, Machi mwaka huu.

“Rais wa CAF pamoja na Waziri Mkuu wa Tanzania kwa pamoja watazungumza kuhusu mpira wa Miguu Tanzania, katika ukanda wa CECAFA na barani Afrika”, ilisema taarifa hiyo.

“Watajadiliana pia kuhusu mashindano ya mashule ya CAF Pan African ambayo bado hayajazinduliwa. Dk. Motsepe alitangaza mwezi Aprili huko Kinshasa” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Motsepe atahudhuria mkutano mkuu wa CECAFA unaofanyika Dar es Salaam katika Hoteli ya Golden Tulip.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends