Rais wa shirikisho la kandanda la Misri abwaga manyanga

Rais wa chama cha mpira wa miguu cha Misri Hany Abou Rida amejiuzulu jana usiku na kuipiga kalamu timu yake ya kiufundi baada ya wenyeji wa Misri kuondolewa katika Kombe la Mataifa ya Afrika. Taarifa ya chama cha kandanda imesema uamuzi huo ni wajibu wa kimaadili baada ya timu ya taifa kuduwazwa kwa kufungwa 1 – 0 na Afrika Kusini, ikiongeza kuwa wanachama wote wa bodi wameombwa kujiuzulu. Amekuwa usukani wa EFA tangu 2016.

Kocha wa Misri Javier Aguirre amesema anabeba lawama kutokana na matokeo hayo ya kushangaza na akadokeza kuwa atafanya mazungumzo na chama cha kandanda cha Misri kuhsu mustakabali wake.

Misri walipigiwa upatu kubeba kombe hilo katika ardhi ya nyumbani lakini ikakutana na Afrika Kusini ambayo ilipena tu katika hatua ya mtoani kupitia nafasi nne za mwisho zilizowekewa timu ambazo zilikuwa bora katika nafasi ya tatu kwenye makundi yao.  Thembinkosi Lorch alifunga bao hilo pekee la ushindi katika dakika ya 85 kwa upande wa Afrika Kusini

Author: Bruce Amani