Rashford airudisha historia mbaya kwa Paris Saint-Germain baada kufunga goli jioni

Mancheater United imeendeleza rekodi nzuri ya ushindi mbele ya Paris Saint-Germain katika michezo inayopigwa dimba la Parc des Princes baada ya mtanange wa leo Jumanne hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa kufanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa ushindi wa goli 2-1. Muuaji wa mtanange huo alikuwa ni yule yule ambaye aliwaua PSG msimu wa 2018/19 ambaye ni Marcus Rashford akitupia bao la dakika za mwishoni kwa shuti kali akimalizia pasi ya kiungo mshambuliaji raia wa Ufaransa Paul Pogba.

Itakumbukwa penati ya dakika za mwishoni miezi 18 iliyopita, Rashford alikwamisha nyavuni katika dimba hilo. Kilikuwa kipindi kizuri zaidi kwa wageni ambao waliotangulia kuliona goli kupitia kwa Bruno Fernandes kwa njia ya penati.

Ungwe ya pili, mabingwa hao wa Ligi Kuu nchini Ufaransa Ligue 1 walikuja kwa nguvu ambapo dakika za mapema walisawazisha bao kupitia kwa bao la kujifunga na strika Anthony Martial.

Akiwa katika ubora mkubwa, kipa wa Kihispania David de Gea amewakatalia wenyeji bao baada ya kusimama imara kwenye mashuti ya Kylian Mbappe na Neymar kwa nyakati tofauti.

Author: Asifiwe Mbembela