RB Leipzig yabanwa na Hertha Berlin kwa sare ya 2 – 2 na kushindwa kuipiku Dortmund

RB Leipzig wamepoteza nafasi ya kukwea mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga baada ya kubanwa mbavu na Hertha Berlin.

Wageni wa mchezo walianza kutangulia kwa goli la Marko Grujic ambaye yupo Hertha kwa mkopo akitokea Liverpool akimalizia mpira wa kona wa Marvin Plattenhard.

Wenyeji wa mtanange huo RB Leipzig walisawazisha kupitia kwa Lukas Klostermann aliyepiga kichwa mashine kwa mpira wa kona pia kabla ya Marcel Halstenberg kuonyeshwa kadi nyekundu.

Hata hivyo, licha ya kuwa pungufu Patrik Schick aliitanguliza Leipzig kwa goli la pili lililofutwa na mshambuliaji wa zamani wa AC Milan na sasa Hertha Krzysztof Piatek kunako dakika za lala salama matokeo kuwa 2-2.

Leipzig walikuwa wanahitaji ushindi ili kuipiku Borrusia Dortmund katika nafasi ya pili kwa tofauti ya goli za kufunga na kufungwa, lakini sare ina maanisha Leipzig wanakuwa nyuma kwa alama mbili ya Dortmund na alama tisa ya Bayern Munich vinara wa ligi ya Bundesliga.

Jumamosi Hertha Berlin ambao wanakamata nafasi ya 10 watapepetana vikali na Augsburg, Jumatatu RB Leipzig watakuwa ugenini kucheza na Cologne.

Katika matokeo mengine ya Jana,

Union Berlin ilitoka sare ya 1 – 1 na Mainz, Hoffenheim ikaibwaga Cologne 3 – 1, Schalke ikalazwa 2 – 1 na Duesseldorf nayo Augsburg ikatoka 0 – 0 na Paderborn.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends