Real Madrid kucheza na Al Ain fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu

61

Mshambuliaji wa Real Madrid Gareth Bale ameifungia klabu yake goli tatu katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Kashima Antlers kwenye mashindano ya kombe la Dunia la Vilabu. Matokeo hayo yanaifanya Madrid kufuzu kucheza mchezo wa fainali ya mashindano hayo dhidi ya Al Ain kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu siku ya Jumamosi Disemba 22.

Bale raia wa Wales alifunga goli la kwanza baada ya mpira kugonga mtambaa wa panya na kuingia wavuni, huku magoli mengine mawili akisaidiwa na Marcelo. Goli la pili lilipatikana kupitia uzembe wa walinzi wa Kashima baada ya kushindwa kuuzuia mpira uliokuwa umerudishwa kwa mlinda mlango kabla ya Bale kuuwai na kufunga goli hilo.

Baada ya Hat trick hiyo sasa, Bale anafikisha goli 6 katika mashindano ya Kombe la Dunia kwenye ngazi ya vilabu lakini hakumaliza mchezo huo baada ya kufanyiwa mabadiliko na kocha Santiago Solari kutokana kusumbuliwa na maumivu madogo ya kifundo cha mguu.

Real Madrid wanategemea kushinda taji hilo mara ya tatu mfululizo baada ya kushinda misimu miwili iliyopita. Mchezo wa fainali utapigwa Abu Dhabi katika uwanja wa Zayed Sports City.

Author: Bruce Amani