Real Madrid yakamata nafasi ya tatu, Atleti yaimulika Barca

Real Madrid imepanda katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi baada ya mabao ya dakika za mwisho kutoka kwa Casemiro na Luka Modric kuwazamisha Sevilla.

Timu hizo mbili hazikuwahi kutoka sare tangu mwaka wa 1993 lakini mechi hiyo ilionekana kuelekea kumalizika kwa sare baada ya Real kupoteza nafasi kadhaa za kufunga katika mechi hiyo walioitawala kwa kipindi kirefu.

Lakini wakati zikisalia chini ya dakika 15, Casemiro alifungua ukurasa wa mabao kwa kusukuma wavuni shuti kali. Modric kisha alitimka kama pikipiki katika dakika za majeruhi na kuhakikisha kuwa Real wanaponyoka na pointi zote tatu muhimu.

Ushindi huo sasa unaifanya Real kuwapiku wapinzani wao kwenye msimamo wa ligi. Wako nyuma ya mahasimu wao wa mjini Atletico Madrid na pengo la pointi tano. Atletico waliwazaba SD Huesca 3 – 0 katika mechi nyingine ya Jumamosi. Atleti sasa wako nyuma ya Barca na tofauti ya pointi mbili tu. Mabeki Lucas Hernandez na Santiago Arias waliiweka Atleti katika udhibiti kabla ya Koke kuhakikisha  kuwa vijana hao wa Diego Simeone wanachukua pointi tatu na kufikisha 17 idadi ya mechi walizocheza mfululizo bila kufungwa kwenye ligi

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends