Real Madrid yapunguza pengo kwa ushindi dhidi ya Alaves

Real Madrid imejitahidi kupunguza mwanya kati yake na Barcelona na Atletico Madrid katika La Liga baada ya Karim Benzema na Vinicius Junior kufunga bao kila mmoja katika ushindi wa wa 3 -0 dhidi za Alaves Jumapili.

Benzema, Vinicius na Gareth Bale walianza pamoja kwa mara ya kwanza na thuluthi mbili ya ushirikiano huo mpya wa ‘BBV’ ulizaa matunda wakati Madrid ikitumia fursa ya Barca kutekwa na Valencia nao Atletico kupoteza dhidi ya Real Betis.

Mariano Diaz, aliyeingia kama nguvu mpya aliongeza la tatu baadaye mchezoni. Madrid sasa huenda wakawapiku Atletico kama watashinda derby yao wikiendi ijayo lakini pengo dhidi ya vinara Barcelona, ambao watakabiliana nao katika Copa del Rey Jumatano, bado ni pointi nane.

“Tutapambana hadi mwisho,” alisema kocha wa Madrid Solari. “Leo kulikuwa na hamu kubwa ya kupunguza pengo.”

Awali, Alvaro Morata alianza katika kikosi cha Atletico lakini mwishowe vijana hao wa Diego Simeone walishindwa kutamba baada ya kunyukwa moja bila na Real Betis.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends